Wednesday 25 2020 Daily Mass - a podcast by St Joseph Cafasso Kingongo Parish

from 2020-03-25T13:38:15

:: ::

MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2020

JUMATANO, JUMA LA 3 LA KWARESIMA


SHEREHE YA KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA


SOMO 1

Isa. 7:10 – 14


Bwana alisema na Ahazi akinena,  Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini  sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka,  wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya  Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka  kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara.  Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita  jina lake Imanueli.


Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI

Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8


(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.


Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,

Masikio yangu umeyazibua,

Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)


Katika gombo la chuo nimeandikiwa

Kuyafanya mapenzi yako,

Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;

Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)


Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,

Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)


Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;

Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.

Sikuficha fadhili zako wala kweli yako

Katika kusanyiko kubwa. (K)


SOMO 2

Ebr. 10:4 – 10


Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo  ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea  tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;  Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa)  niyafanye mapenzi yako, Mungu.

Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo  na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa  nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama,  nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi  alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa  mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.


Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO

Yn. 1:14


Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.


INJILI

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa  Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa  na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni  Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema.  Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake,  akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia,  Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua  mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa  mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi  cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme  wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno  hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu  atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli;  kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa  Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto  mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa  tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema,  Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha  malaika akaondoka akaenda zake.


Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Further episodes of St. Joseph Cafasso King'ong'o Parish

Further podcasts by St Joseph Cafasso King'ong'o Parish

Website of St Joseph Cafasso King'ong'o Parish